KILIMO CHA VITUNGUU





UTANGULIZI
Vitunguu maji kwa kitaalamu hujulikana kama Allium cepa na kwa kiingereza huitwa Bulb Onions. Vitunguu ni zao muhimu sana sio kwa matumizi ya ndani tu lakini pia ni zao la kibiashara linaloweza kukuletea kipato kikubwa.   Vitunguu ni zao la bustani  (Horticultural crop) ambalo lipo kwenye kundi la mboga mboga (vegetables).

Zao hili ni maarufu kutokana na thamani ya virutubisho ilivyonavyo na ladha yake kwenye mapishi ya vyakula mbalimbali. Vitunguu ni zao la pili ambalo hutumika karibu kila siku katika mlo wa familia za kitanzania. Afrika Mashariki, na Dunia Nzima.

MATUMIZI YA VITUNGUU

Vitunguu hutumika katika kutengeneza kachumbari, kiungo cha mboga, nyama na samaki. Majani ya kitunguu hutumika kama mboga. Vitunguu pia hutumika kutengeneza supu n.k

KILIMO

Nchini mwetu vitunguu hulimwa kwa wingi katika mikoa ya Tanga,  Arusha sehemu za Mang’ora na Babati, Kilimanjaro, Singida, Morogoro, Iringa wilaya ya Kilolo mpakani mwa mkoa wa Morogoro na kwenye maeneo ya mto Ruaha , Mara , Morogoro wilayani Kilosa sehemu za Lumuma na Malolo ,Mbeya Kilimanjaro na baadhi ya sehemu za Mkoa wa Singida.

Katika shamba lililo hudumiwa vizuri na kupandwa katika hali ya hewa na aina ya mbengu. Vitunguu hutoa kiasi cha tani (10) hadi 16 kwa ekari moja.

Zao hili hulimwa katika nchi nyingi za magharibi, nchi za milima zilipo kaskazini mwa dunia, likwemo bara la Afrika. Vitunguu hustawi katika hali ya hewa ya jotoridi 13°C – 24°C, hali ya hewa inayofaa kwa kuotesha na kukuzia miche kwenye kitalu ni jotoridi 20°C – 25°C. Kwa kawaida vitunguu huhitaji kiasi cha joto nyuzi 20°C-25°C ili kuweza kustawi na kukua vizuri. Joto zaidi ya hapo hufanya vitunguu kudumaa na kutoweza kutengeneza viazi (bulbs).

AINA ZA VITUNGUU
Vitunguu maji vimegawanyika katika makundi matatu:
KUNDI LA KWANZA: VITUNGUU VYEUPE (WHITE ONIONS).  Vitunguu hivi ni vyeupe nje na nadni pia: Mfano ni White granex, snow white

KUNDILA PILI: VITUNGUU VYA NJANO (YELLOW ONIONS).
Vitunguu hivi hua na rangi ya dhahabu kwa nje, ila ndani nyama yake ni ya njano mpauko.  Vitunguu hivi ni vitamu (ladha ya sukari) kuliko aina nyingine ya vitunguu. Mfano: Texas Supersweet, Walla Walla Sweet, Granex Yellow Hybrid, Candy Hybrid

KUNDI LA TATU: VITUNGUU VYEKUNDU (RED ONIONS):
Hivi vina rangi nyekundu kwa nje na ndani kunakua na rangi nyeupe. Mfano  Red Creole, Red Bombay, Neptune F1, Tajirika, Meru Super, Mang’ola Red, JAMBAR F1, n.k Aina hizi za vitunguu vyekundu ndizo hupendwa zaidi na walaji na ndio huzalishwa kwa wingi. Hivyo katika mafunzo yetu tutajikita zaidi kwenye aina hizi za vitunguu vyekundu.

AINA ZA MBEGU ZA VITUNGUU
Kuna aina tatu za mbegu za vitunguu.AINA YA KWANZA: MBEGU ZA KIENYEJI:   Hizi ni zile mbegu zinazozalishwa na wakulima wenyewe. Mara nyingi mbegu hizi zinakua hazijathibitishwa na wataalamu kutoka taasisi ya kuthibiti ubora wa mbegu (TOSCI). Wakulima wanazalisha mbegu hizi na kuwauzia wakulima wengine kwa kutumia kipimo cha kilo au debe.

Wakulima wengi hupendelea mbegu hizi za kienyeji kwa vile bei yake ni ndogo. Mbegu hizi maeneo mengi huuzwa kati ya 20,000 hadi 30,000 kwa Kilo moja ya mebgu.  Kutokana na kwamba mbegu hizi zina ubora mdogo, mkulima inambidi atumie mbegu nyingi ili kutosheleza mahitaji ya ekari moja.

Kwa ekari moja mkulima hutumia kilo 6 hadi 10 za mbegu hizi ili kutosheleza. Kama mtaalamu wa kilimo simshauri mkulima anayetaka kulima kibiashara kutumia mbegu hizi za kienyeji kwa maana hata Mavuno yake hayatabiriki. Ila Sio kwamba mbegu zote zinazozalishwa na wakulima ni mbaya, hapana.

Upo utaratibu wa wakulima kuzalisha mbegu kitaalamu kwa kufuata utaratibu ulipo kisheria. Mbegu hizo zinazozalishwa na wakulima kitaalamu huitwa mbegu za daraja la kuazimiwa (quality declared seeds) au kwa kifupi huitwa QDS. Mbegu hizi za QDS zina mipaka yake ya eneo la kutumika.


Na wazalishaji wa QDS lazima wapate mafunzo na wasajiliwe na Taasisi ya Uthibiti Ubora wa Mbegu (Tanzania Official Seed Certification Institute) au kwa kifupi TOSCI. TOSCI pia wana utaratibu wa kufanya ukaguzi na kutoa kibali cha mbegu hizo za QDS kuuzwa kama zimekizi vigezo husika. Kama hazijakizi mbegu hizo haziruhusiwi kuuzwa kwa wakulima.

AINA ZA KILIMO CHA VITUNGUU
Kilimo cha vitunguu kinaweza kufanyika kwa aina mbili;

Green House -Vitunguu hulimwa ndani ya green house ili kuongeza uthibiti wa joto hali ya hewa wadudu, magonjwa na mwanga wa jua.

Shambani (field)- vitunguu hulimwa wazi katika shamba ambalo limeandaliwa


HALI YA HEWA INAYOFAA KWA KILIMO CHA VITUNGUU
Zao la vitunguu hustawi vizuri kwenye maeneo yasiyo na mvua nyingi sana, yenye baridi kiasi wakati wa kiangazi na yasiyo na joto kali pamoja na ufukuto wa ukungu wakati wa kukomaa vitunguu.

UDONGO

  Zao la vitunguu hustawi vizuri kwenye udongo wenye rutuba ya kutosha. Udongo unao ruhusu mizizi kupenya kirahisi, unao hifadhi unyevu kama vile udongo wa mfinyanzi tifutifu. Sehemu nyingi zinazostawi vitunguu maji hufaa pia kwa zao hili. Maeneo ya mwinuko wa kiasi cha zaidi ya mita 1000 juu ya usawa wa bahari hufaa zaidi.

KUTAYARISHA SHAMBA
Lima shamba kwa trekta, kwa ng’ombe ama kwa jembe la mkono kwa kina cha sentimita 30 hadi 45 Weka matuta ya mwinuko yenye upana wa mita 1 hadi mita 1.5 kutoka kati kati ya tuta na tuta na upana wa mita 1 Lainisha udongo au kwa kitaalamu inaitwa Harrowing. Yaani yale mabonge makubwa makubwa ya udongo yanagongwa na kutengneza udongo mlaini. Harrow ifanyike wiki 2 au 3  baada ya kulima.

Zipo trekta zinazofungwa mashine ya kufanya harrowing. Shamba litayarishwe sehemu usiyokuwa na mwinuko, sehemu ya wazi ambayo haijalimwa vitunguu kwa muda wa miaka 2 -3. Shamba liwe karibu na chanzo cha maji kwa ajili ya umwagiliaji. Matutu au majaruba yanarahisisha umwagiliaji, palizi na unyunyiziaji wa dawa.

UPANDAJI WA MBEGU ZA VITUNGUU
Vitunguu vinaweza kupandwa kwa njia mbili:

 NJIA YA KWANZA:  UPANDAJI WA MOJA KWA MOJA (DIRECT PLANTING).
Namna ya Kupanda vitunguu kwa njia ya moja kwa moja: Andaa shamba vizuri, udongo uwe mlaini, usiwe na mabongemabonge ya udongo. Weka  mbolea ya samadi kwa kutawanya (broadcasting) kisha ichanganye vizuri na udongo.

Mbolea ya samadi inayotosha kwa ekari moja ni tani 16. Baada ya kuchanganya vizuri samadi kwenye udongo, tengeneza mistari (drills) yenye kina cha sentimita 2.5 na yenye umbali wa sentimita 30 kutoka mstari hadi mstari.

NJIA YA PILI: UPANDIKIZAJI WA MICHE (TRANSPLANTING).
Hapa Miche inakuzwa kwenye kitalu kwa wiki 6 hadi 8 tangu kisia mbegu kisha inahamishiwa shambani. Inakadiriwa kwamba wiki 6 hadi 8 miche itakua imefikia kiwango kizuri cha ukuaji kwa ajili ya kuhamishiwa kwenye shamba kuu (main field).

Hii ndio njia inayoshauriwa zaidi na ndiyo inayotumia na wakulima wengi wa vitunguu. Hapa Tanzania upandaji wa mbegu za vitunguu katika kitalu kwa ujumla huanza mwezi machi hadi mei kutegemea na msimu wa kilimo.

Hivyo kilimo hiki hufanyika mara baada ya mvua za masika kubwa kuisha. Kipindi cha kiangazi na baridi huruhusu ukuaji mzuri wa vitunguu. Mbegu za vitunguu huoteshwa mapema katika kitalu. Mbegu zinaweza kupandwa kwa mstari au kwa kutawanya katika tuta la kitalu. Katika upandaji wa mstari, mbegu hupandwa katika nafasi ya cm 10 hadi 15 kati ya mstari na mstari.

Baada ya kupanda, mbegu hufunikwa kwa udongo na baadaye kwa kuweka matandazo juu ya tuta. Mara baada ya mbegu kuota, matandazo yaondolewe na badala yake kichanja cha nyasi kijengwe ili kuiwekea kivuli mimea michanga. Mbegu huota baada ya siku 7 hadi 10.

UPANDIKIZAJI WA VITUNGUU.
Vitunguu vinapsawa kupandikizwa wakati wa asubuhi au au jioni. Wakati wa jioni ndio mzuri zaidi wa kuhapandikiza miche. Miche inapaswa kupandwa kina kilekile kama ilivyokua kwenye kitalu. Yaani mche unapong’olewa kwenye kitalu kuna sehemu ilikua chini ya ardhi.
Nafasi ya upandaji iwe umbali wa sentimita 30 kati ya mstari na mstari na sentimeta 8 kati ya mche na mche

MATUNZO YA BUSTANI YA VITUNGUU
PALIZI
Mmea wa kitunguu una mizizi mifupi, hii husababisha kutunguu kuathirika sana na ushindani na magugu. Mizizi mifupi ina maana huufanya kukosa uwezo wa kustahimili ushindani wa magugu.

Magugu yana uwezo mkubwa wa kufyonza virutubisho ardhini kuliko mimea ya mazao, na ndio maana magugu hukua kwa haraka kuliko mazao.  Hivyo inashauriwa katika shamba la vitunguu hakikisha unafanya palizi kwa wakati.

Idadi ya palizi inategemea na aina na wingi wa magugu wa eneo husika. Kwenye ameneo yenye magugu mengi, palizi hufika hadi 4, na kwa maeneo ambapo magugu sio tatizo palizi mbili zinatosha.

Kuna mbinu mbalimbali za kfuanya palizi kama matumizi ya dawa za kudhibiti magugu (herbicides), palizi ya mkono (hand weeding) na uwekaji wa matandazo (mulching).

UMWAGILIAJI
Zao la vitunguu linahitaji maji ya kutosha katika kipindi chote cha ukuaji wa mmea na hasa wakati wa kutunga tunguu. Katika kipindi kisicho na mvua (mwezi mei hadi Agosti) Umwagiliaji ufanyike mara moja kwa wiki kwa udongo wa mfinyanzi tifutifu na vitunguu vilivyopandwa katika vijaruba.

Ili kuharakisha kukomaa kwa vitunguu unashauriwa kupunguza kiasi cha maji ya kumwagilia taratibu kadri zao linavyo kua. Pia ni vizuri uache kumwagilia maji mapema wiki nne hadi sita kabla ya kuvuna. Kwani muda kamili wa kukomaa na kuvuna kwa vitunguu ni siku 90 hadi 150 kutegemea na aina ya mbegu.

Kuthibiti magugu na kupandishia udongo Kitunguu ni zao lisilo weza kushindana na magugu. Magugu husababisha kupungua kwa ukubwa wa kitunguu, hueneza magonjwa na husababisha kudumaa kwa vitunguu. Katika bustani ya vitunguu, magugu yanaweza kutolewa kwa njia ya kutifulia kwa jembe dogo, kung’olea kwa mkono na pia kwa kutumia madawa ya kuua magugu.

Kama unaondoa magugu kwa kutifulia, epuka kutifua kwa kina kirefu ili kutoharibu mizizi na vitunguu vyenyewe, kwani mizizi ya vitunguu ipo juu juu sana. Kupandishia udongo kwenye mashina ya vitunguu ni hatua muhimu ili vitunguu visiunguzwe na jua. Hakikisha kuwa mashina ya vitunguu vyako ndani ya udongokama sentimita 5.

Pia kuna aina ya vitunguu ambavyo hutoa au hupandisha tunguu lake juu ya udongo wakati vinapokua. Hivyo kupandishia udongo ili kufunika tunguu ni muhimu sana.

UVUNAJI WA VITUNGUU
Muda wa ukomaaji wa vitungu hutegemea aina ya vitunguu pamoja na hali ya hewa ya eneo husika. Aina za chotora  (hybrid) mara nyingi hukomaa mapema, huchukua miezi 3 hadi 5 baada ya kusia mbegu. Aina za kawaida (OPV) na zile za kienyeji hazina ukomaaji unaofanana (do not mature uniformly), hukomaa kwa makundi makundi.

Pia mara nyingi hukomaa miezi 4 na kuendelea kuanzia kusia mbegu. Kama shamba lako unatumia umwagiliaji, basi umwagiliaji unapaswa kukoma siku 7 hadi 10 kabla ya kuvuna. Uvunaji unaanza pale majani ya vitunguu yanapoanza kukauka, kupoteza rangi na kujikunja.

Yale majani ya nje yanayofunika kitunguu unene wake unapungua. Hizo ndio dalili za kitunguu kua tayari kwa kuvunwa. Uvunaji wa mapema (early harvest) hupelekea vitunguu ambavyo havijakomaa vizuri, hivyo kusababisha kupoteza maji na  kusinyaa kwa vitunguu wakati wa ukaushaji wa vitunguu.

Pia uvunaji wa kuchelewa (late harvest) husabisha kitunguu kupoteza rangi yake, kuoza kwa yale maganda/majani yanayokua yamekifunika kitunguu chenyewe (onion bulb). Hivyo basi kitunguu kinapaswa kuvunwa kwa wakati sahihi ili kuepuka hasara inayoweza kutokana na kuwahi au kuchelewa katika uvunaji.

Wakati wa uvunaji, vitunguu hung’olewa toka ardhini, kisha kukatwa mizizi yake ili kuzuia ukuaji wa majani. Baada ya hapo ukaushaji wa vitunguu unaanza.

UKAUSHAJI WA VITUNGUU.
Baada ya kuvuna kitunguu, hatua inayofuata ni ukaushaji (curing) na hii inafanyikia palepale shambani. Kukausha kitunguu ni ule mchakato wa kukausha ile shingo ya kitunguu. Shingo ya kitunguu inapokauka inakifunga kitunguu, pia inaziba njia ambazo zinaweza kutumiwa na vijidudu kuingia ndani kuharibu kitungu.

Ukaushaji pia husaidia kupata kitunguu chenye ngozi iliyokauka na yenye rangi nzuri. Ngozi tunamaanisha lile ganda la nje lililofunika kitunguu.  Baada ya kung’olewa vitunguu shambani unavikusanya kwenye makundi makundi, kisha hayo makundi ya vitunguu unayafunika na majani makavu ili kuepuka kuchomkea na jua na kutengeneza mabaka ya kuchomwa na jua (Sunscald).

Muunguzo wa jua (sunscald) yaani kitunguu kinapopigwa na mionzi ya jua huua au huharibu lile ganda la nje na hivyo kupelekea kitunguu kuwa na muundo usiofaa au kuvutia vijidudu vyenye kusababisha kitunguu kuoza. Viache vitunguu kwa muda wa wiki moja au mbili ili vikauke vizuri, kisha vipakie kwenye magunia kwa ajili ya kwenda kuhifahi au kwa ajili kupeleka sokoni.

UHIFADHI WA VITUNGUU (STORAGE)
Kitungu ndio zao lenye uwezo wa kuhifadhika kwa muda mrefu zaidi kuliko mazao yote ya mboga mboga. Kitunguu baada ya kuvunwa bado kinakua ni kiumbe kinachoishi (living organism) ikimaanisha kinaenelea na michakato kama kupumua, kupoteza maji n.k Hivyo uhifadhi wake unahitaji umakini ili kuweza kukaa muda mrefu bila kuharibika.

Hii ni tofauti na mazao kama mahindi, maharage n.k, ambapo yakishakaushwa yanabaki na asimilia ndogo sana ya unyevunyevu, na unaweza kuyaweka kwenye pipa au dramu na ukafunika na kuziba kabisa bila kua na hata hewa, na mahidni yakaendelea kukaa salama kabisa. Ila kitunguu ni tofauti, kikikosa hewa kinaharibika. Mbinu na mifumo mizuri ya uhifahi wa kitunguu ni muhimu sana kwa ubora wa vitunguu utakao kubalika katika masoko.

Comments

Popular posts from this blog

UFUGAJI BORA WA NGURUWE

UFUNGAJI WA KUKU WA MAYAI