KILIMO BORA CHA NYANYA



KILIMO BORA CHA NYANYA

1.0 UTANGULIZI
Nchini Tanzania zao la nyanya hulimwa karibu katika mikoa yote hasa ya Arusha, Kilimanjaro, Morogoro, Iringa, Mwanza, Dodoma, Tanga, Pwani na Mbeya.

Nyanya ni zao la chakula na
biashara.

Kilimo cha zao hili hufanyika majira yote (masika na kiangazi), na faida hupatikana
haraka na ni ya kuridhisha ikilinganishwa na mazao mengine.

Pamoja na umuhimu wa zao hili, wadudu waharibifu na magonjwa huathiri uzalishaji na ubora wa matunda.

Ili mkulima aweze
kupata faida na kuongeza pato la kaya yake ni vema kuzingatia kanuni bora za kilimo pamoja na
udhibiti wa magonjwa na wadudu wa zao hili.

Kwa manispaa ya Musoma zao la nyanya hulimwa na wakulima hulitegemea zao hili kama zao
la biashara kwa kuwa huwapatia faida kubwa ukilinganisha na mazao mengine ya mbogamboga.

Halmashauri ya Manispaa ya Musoma imelipa kipaumbele zao hili kwa kulichagu zao hili na
kuliweka kwenye mnyororo wa thamani kwa kutoa mafunzo ya kilimo bora cha zao la nyanya ili
wakulima waweze kulima zao hili kwa tija.

.1.1 FAIDA YA NYANYA
-Nyanya hutupatia vitamini A, B, na C. pia zina madini aina ya chuma na chokaa. -Nyanya hutumika zaidi kama kiungo na ni chakula. -Nyanya hutupatia pesa (Ni zao zuri kwa biashara)

1.2 MATUMIZI:
Nyanya hutumika kama kiungo cha kupikia. Huweza kuliwa mbichi kama kachumbari au zikiwa
zimekaangwa pamoja na nyama au mboga yoyote.

Nyanya pia zinaweza kutengenezwa supu, vinywaji, achari, jemu, sosi na pesti.

Vilevile zinaweza kukatwa katwa vipande na kuhifadhiwa
kwenye makopo.

Mabaki ya mimea hutumika kama mbolea na chakula cha wanyama.

1.3 MAZINGIRA:

Udongo
Nyanya hustawi kwenye aina zote za udongo kuanzia udongo wa kichanga, mwepesi na
tifutifu hadi udongo wa mfinyanzi, ili mradi uwe na mboji ya kutosha.

Udongo unaofaa
zaidi ni ule wa kitifutifu na wenye mboji nyingi.

Hali kadhalika udongo wenye uchachu
wa wastani yaani pH 6.0 - 7.0 ni mzuri kwa kilimo cha zao hili.

Hali ya Hewa
Nyanya hustawi vizuri zaidi kwenye mazingira ya joto la wastani kuanzia nyuzi joto 18-30
sentigreti.

Mvua nyingi husababisha mlipuko wa magonjwa ya ukungu kama vile Baka jani
chelewa n.k.) Joto likizidi husababisha matawi ya matunda kuwa machache.

Vilevile joto
jingi, mwanga kidogo, pamoja na hali ya unyevunyevu husababisha magonjwa mengi
kuenea na mmea kuwa na majani mengi na matunda kidogo.

Joto kidogo hufanya mimea
kutoa matawi mengi na matunda madogo ambayo huchelewa kukomaa.
Zao hili hupendelea mvua za wastani pamoja na kipindi kirefu chajua.
Hali ya mvua nyingi pamoja
na baridi kali husababisha kuenea kwa magonjwa na wadudu waharibifu.

2.0 AINA ZA NYANYA:
Aina nzuri za nyanya ni zile zinazotoa mavuno mengi na bora; zinazostahimili magonjwa, zinazokomaa mapema, zenye ladha nzuri na umbo la kuvutia,.

Zifuatazo ni aina bora za nyanya
zinazolimwa hapa nchini; Aina hizi zimegawanyika katika makundi makuu mawili kutegemea
ukuaji wake.

2.1 Kutokana na tabia ya ukuaji, nyanya zinagawanyika katika makundi
mawili:

1.Aina ndefu ( intermediate) kwa mfano ANNA F1, Tengeru 97. Money Maker, Marglobe, Beef
Master, Lot No 2009, Mandel na Tanya.
Aina hizi hufanya vizuri zaidi zinapopandwa ndani ya
greenhouse. Uvunaji wake ni wa muda mrefu, zipo ambazo zinavunwa hata zaidi ya miezi 6, yaani hiyo miezi 6 ni ya uvunaji.

2. Aina fupi (determinate) kwa mfano Tanya, Cal J, Mwanga, Onyx, Roma VF (nyanya
mshumaa), Dwarf germ, Amateur, Red Cloud, Reza na Columbian.

2.2 Kutokana na uchavushaji, nyanya zinagawanyika makundi mawili:

1. OPV (Open Pollinated Variety) - Aina za kawaida

2. Hybrid – Chotara:
Hizi ni aina zenye mavuno mengi, kati ya hizo zipo aina fupi na ndefu. Katika karne hii ya 21, nyanya zinazopendelewa kulimwa zaidi na wakulima, ni zile zinazoweza
kuvumilia magonjwa, zinazo zaa sana, na zenye ganda gumu ili kufanikisha usafirishaji, na
kuhifadhika kwa siku nyingi bila kuharibika mapema.

3.0 Kuandaa Kitalu cha Nyanya

3.1 Mambo muhimu ya kuzingatia

• Kitalu kiwe karibu na maji ya kutosha na ya kudumu

• Kiwe sehemu iliyowazi na yenye udongo ulio na rutuba ya kutosha

• Eneo la kitalu kama ni kubwa liwe tambarare au na mwiinuko kidogo ili kuepuka maji
yasituame kwenye kitalu,
mtelemko ukiwa mkali sana nao sio mzuri kwani husababisha
mmomonyoko wa udongo.

• Kitalu kiwe sehemu ambayo haikuwa na zao la nyanya au viazi mviringo (au mazao ya jamii
ya nyanya k.m. mnavu, biringanya n.k.)

• Kiwe sehemu ambayo ni rahisi kupata huduma zote muhimu kwa urahisi, ikiwa ni pamoja na
uhamishaji wa miche kwenda sehemu nyingine. Pia kurahisisha usambazaji wa miche kwenda
sehemu nyingine.

3.2 Kuandaa Matuta ya Kusia Mbegu za Nyanya.

Aina ya matuta:
– matuta ya makingo (sunken seed bed)

– matuta ya kunyanyulia udongo (raised seed bed)

– matuta ya kawaida (flat seed beds)


3.3 Mambo Muhimu ya Kuzingatia wakati wa Kuandaa Matuta

• Tuta liwe na upana kati ya sentimita 90-120, na urefu wowote, [ili mradi muhudumu anaweza
kutoa huduma nyingine zote kitaluni bila kukanyaga miche].

• Kwatua/lima kina kirefu cha kutosha kiasi cha sentimita 15-20 ili mizizi iweze kusambaa vizuri
ardhini.

• Choma takataka juu ya kitalu, au funika tuta kwa nailoni, majuma 4-8 ili kuua vimelea vya
magonjwa na wadudu.

• Wakati wa kuandaa, kitalu, ongeza mbolea aina ya samadi/vunde au mboji kwenye udongo
kisha kwatua ili ichanganyike vizuri na udongo.

• Changanya kiasi cha debe 1 hadi 2 kila baada ya mita moja (hatua moja) mraba.

• Tuta lisiwe na mabonde mabonde au mawe mawe ambayo yanaweza kuzuia usambaaji mzuri
wa mbegu kwenye tuta, lisawazishwe vizuri ili kuhakikisha usambazaji mzuri wa mbegu na
kuepuka mbegu kufukiwa chini mno kiasi ambacho hazitaota.

4.0 KUOTESHA/KUSIA MBEGU:

Mwagilia kitalu siku moja kabla ya kupanda, kisha sia mbegu katika mistari yenye nafasi ya
sentimita 10 hadi 20 kutoka mstari hadi mstari Kina cha mistari kisiwe cha kutisha bali kiwe
kati ya sentimita 1-2.
Matuta yapate maji ya kutosha siku moja kabla ya kusia mbegu.
Ni vizuri
kutumia chombo cha kumwagilia (watering can).
Kiasi cha mbegu kitakachotosha eneo hilo la
mita mraba moja ni gramu tatu hadi tano (sawa na nusu kijiko cha chai mpaka kijiko kimoja).
Kiasi hiki cha mbegu huweza kutoa miche inayoweza kutosha kupandikiza katika eneo la mita
mraba 100.
Kiasi cha mbegu kinachohitajiwa kwa hekta moja ni gramu 300 hadi 500.
Mbegu ziatikwe kwenye mistari na zisambazwe vizuri ili kufanikisha usambaaji mzuri wa
mbegu kwenye tuta.
Changanya mchanga laini na mbegu kisha sambaza kwenye mistari
iliyoandaliwa kwenye tuta.
Mbegu zinaweza pia kuatikwa kwenye tuta bila mistari, lakini zisambazwe kwa uwiano mzuri
kwenye tuta ili kupunguza msongamano.
Msongamano husabisha magonjwa ya fangasi kama
vile kinyausi (damping off) au ukungu (blight).

• Weka matandazo kama vile nyasi kavu au majani ya migomba kiasi cha kutosha ambacho
hakitazuia kuota kwa mbegu.

• Mara baada ya kusia mbegu, mwagilia maji kiasi cha kutosha kulingana na unyevu nyevu
ulioko ardhini endelea kisha mwagilia maji asubuhi na jioni mpaka mbegu zitakapoota.
Mbegu
huota baada ya siku tano hadi 10.
Ondoa nyasi mara baada ya mbegu kuota.
Jenga kichanja ili
kuzuia jua kali na matone ya mvua yanayoweza kuharibu miche .

4.1 Mambo ya Kuzingatia baada ya kusia mbegu pamoja na Matunzo
Kitaluni

• Punguzia miche (thinning) ili ibakie kwenye nafasi ya kutosha.
Hivyo miche ibakie kwenye
umbali wa sentimita 2.5 - 4. Hii itapunguza magonjwa ya ulemavu na mnyauko, pia itasaidia
kupata miche bora na yenye nguvu.

• Endelea kumwagilia hadi miche ifikie kimo kinachofaa kuhamishia shambani.

• Punguza kiwango cha umwagiliaji maji, siku chache kabla ya kuhamishia miche shambani, yaani siku 7-10.


5.0MAANDALIZI YA SHAMBA LA NYANYA

• Shamba la nyanya liandaliwe mwezi 1-2 kabla ya kupanda miche.

• Katua ardhi katika kina cha kutosha hadi kufikia sentimita 30.
Lainisha udongo kwa kuvunja
mabonge makubwa kwa kutumia jembe. Mara baada ya kulima choma nyasi juu ya udongo au
ondoa magugu yote yanayoweza kuhifadhi wadudu na magonjwa ya nyanya.

•. Weka mbolea za asili wiki mbili kabla ya kupandikiza.
Kiasi kinachohitajika m tani 20 kwa
hekta (sawa na ndoo moja hadi mbili) kwa kila eneo la mita mraba mmoja.
Mbolea hii iwekwe
katika kila shimo la kupandia na ichanganywe vizuri pamoja na udongo.
Siku moja au mbili
kabla ya kuhamishia nyanya shambani, mwagilia sehemu iliyoandaliwa kwa ajili ya kuhamishia
nyanya

5.1Mbinu za kuhamisha miche toka Kitaluni kwenda shambani (Transplanting)
Rules)

• Mwagilia miche masaa machache kabla ya kuhamishia miche shambani ili wakati wa kung’oa
miche mizizi ishikamane vizuri na udongo.

• Kabla ya kuhamisha miche, mashimo yawe yamekwisha andaliwa katika nafasi zinazo stahili
huko shambani.

• Miche ihamishwe wakati wa jioni ili kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na jua.

• Kwa ujumla karibu mazao yote ya mboga mboga huwa tayari kuhamishiwa shambani yakiwa
na majani kamili kati ya 2-6 pamoja na mizizi mingi iliyostawi vizuri.

• Mche lazima uwe na afya nzuri, uwe umenyooka vizuri, hivyo miche yote iliyonyongea au
myembamba kupita kiasi isichukuliwe wakati wa kupeleka shambani.

• Ng’oa miche kwa uangalifu hasa pamoja na udongo wake kwa kutumia vifaa husika ili mizizi
isidhurike.

• Miche ihamishiwe shambani mapema mara baada ya kung’olewa toka kitaluni.

• Wakati wa kuhamisha miche, uangalifu mkubwa utumike ili kutoharibu miche/mizizi.

6.0 KUPANDIKIZA:
Upandikizaji wa miche shambani hufanyika baada ya wiki nne hadi sita kutegmea hali ya hewa.
Siku 10 hadi 14 za mwisho kabla ya kupandikiza, izoeshe miche hali ngumu ambayo inalingana
na ile ya shamba la kudumu.
Wakati huu ipatie miche maji kidogo na iondolee kivuli.
Mwagilia kitalu siku moja kabla ili kurahisisha ung'oaji wa miche na kuepuka kukata mizizi.
Pia ni muhimu kumwagilia shamba siku moja kabla ya kupandikiza. Iwapo mbolea za asili
hazikutumika wakati wa kutayarisha shamba unashauriwa kuweka mbolea ya mchanganyiko
(N.P.K. 5:10:5) kiasi cha gramu tano kwa kila shimo wakati wa kupandikiza.

6.1 Jinsi ya kupanda miche:

• Hamisha miche toka kitaluni pamoja na udongo wake

• Sambaza mizizi vizuri kwenye shimo bila kukunja.

• Fukia miche kina kile kile ambacho shina lilikuwa limefukiwa bustanini.

• Mwagilia maji ya kutosha kulingana na unyevunyevu uliopo kwenye udongo kisha weka
matandazo na kivuli ili kupunguza uharibifu unaosababishwa na mionzi ya jua.

•Pandikiza miche wakati wa asubuhi au jioni ili kuepukajua kali linaloweza kunyausha miche.
Wakati wa kupandikiza hakikisha mizizi haipigwi na jua, kwa kuiweka katika ndoo au chombo
chochote chenye udongo wenye unyevu.
Pandikiza miche katika kina cha sentimita mbili hadi
tatu zaidi ya ilivyokuwa kwenye kitalu ili kupata mizizi mipya.
Kisha shindilia udongo vizuri
kuzunguka mche na mwagilia maji.

6.2 Nafasi

Nafasi kati ya mche hadi mche ni wastani wa sentimita (50-60) x (50-75) kutegemeana na aina
au hali ya hewa.
Kama ni kipindi cha baridi ni vyema nyanya zikapandwa mbalimbali ili
kuruhusu mzungungo wa hewa na kuzuia magonjwa ya fangasi
Kutokana na nafasi zinazotumika hupandikiza miche shambani hutegemea aina ya nyanya, njia
ya kumwagilia na hali ya hewa,

kwa mfano:- Aina fupi ya nyanya hupandikizwa katika nafasi ya sentimita 90 kutoka mstari hadi mstari, na
sentimita 50 kutoka mche hadi mche.
Nafasi kati ya tuta na tuta iwe sentimita 60.
Aina hii haihitaji kuegeshwa mwenye miti.
Kutokana na nafasi hii jumla ya mimea 240 hadi 275 itaweza
kupandikizwa katika eneo la mita mraba 100 (hatua kumi kwa kumi) ambayo ni sawa na miche
20,000 hadi 22,000 kwa hekta.

6.3 Aina ndefu ya nyanya inayohitaji kuegeshwa kwenye mti hupandikizwa
katika nafasi zifuatazo:-

6.3.1 Kupandikiza Safu Mbili Katika Tuta Moja

Kutoka mstari hadi mstari ni sentimita 75 na mche hadi mche ni sentimita 50 hadi 60.
Aina hii inahitaji kuegeshwa kwenye miti.
Jumla ya mimea 220 hadi 275 inaweza kupandikizwa katika
eneo la mita mraba 100 ambayo ni sawa na miche 18,000 hadi 22,000 kwa hekta.

6.3.2 Kupandikiza Safu Moja Katika Tuta Moja

Nafasi kati ya tuta na tuta ni sentimita 90 na kutoka mche hadi mche ni sentimita 40 mpaka 50.
Jumla ya mimea 220 hadi 275 inaweza kupandikizwa katika eneo la mita mraba 100.

6.3.3 Mambo muhimu ya kuzingatia baada ya kuhamishia Miche Shambani

• Kagua shamba mara kwa mara ili kujua maendeleo au matatizo yaliyoko shambani mapema

• Hakikisha shamba ni safi wakati wote, palilia shamba na hakikisha magugu yote hasa yale ya
jamii ya nyanya yamelimiwa chini.

• Ondoa mimea iliyoshambuliwa na magonjwa au ondoa sehemu zilizoshambuliwa, kisha
zifukiwe chini au kuunguza moto.

• Punguza matawi na vikonyo ili kuongeza mwanga wa kutosha kwenye nyanya pamoja na
kuruhusu mzunguko wa kutosha wa upepo na kusababisha mazingira magumu ya wadudu
maadui kwenye nyanya, hasa wale wanaopenda kiza na magonjwa yanayopendelea unyevunyevu

7.0 KUTUNZA SHAMBA:

7.1 Kuweka Matandazo:

Baada ya kuhamishia miche shambani, weka matandazo ili kuhifadhi unyevu na kuzuia magugu. Matandazo pia husaidia kuzuia mmomonyoko wa udongo na kutunza rutuba.
Vile vile hupunguza uzito wa matone ya mvua na kuweka matunda katika hali ya usafi.

7.2 Kusimika Miti na Kuegesha Mimea:

Kazi ya kusimika miti na kuegesha mimea hufanyika wiki ya pili baada ya kupandikiza.
Miti ya kuegesha mimea iwe imara, na ambayo haiozi haraka.
Simika miti kiasi cha umbali wa sentimita tano kutoka kwenye mmea.
Wakati wa kusimika mti hakikisha kwamba mmea unakuwa upande
wa ndani ili kuzuia mmea usiumie wakati wa kuchuma au kunyunyuzia dawa.
Kisha kwa kutumia mkono shindilia mti sentimita 20 hadi 50 kwenda chini ya ardhi.
Mti uwe na urefu wa
mita moja na nusu hadi mbili na unene wa sentimita mbili hadi tatu.

7.3 Kufunga Nyanya Kwenye Mti
Aina ndefu ya nyanya ni lazima ifungiwe kwenye mti ili kuzuia mmea usitambae chini.
Mimea iliyofungwa kwenye mti hurahisisha unyunyiziaji wa dawa, umwagiliaji na uchumaji wa
matunda.
Ili kupata mazao yaliyo bora na makubwa ondoa matawi yote na kuacha mashina mawili.
Yafungie mashina hayo kwenye mti ili mimea iweze kutambaa na kuwa wima.
Funga kamba katika umbo la nane chini ya kila jani la tatu na kila baada ya sentimita 20 hadi 25.

7.4 Kupunguza Matawi
Kupunguza matawi ni muhimu na hasa kwa aina ndefu kama vile Money Maker.
Kazi hii hufanyika mara moja kwa wiki.
Wakati mzuri wa kupunguzia ni asubuhi.
Ondoa matawi yote na acha shina moja au mawili.
Usitumie kisu kupunguzia matawi hali matawi yavunjwe kwa kutumia mkono.
Utumiaji wa kisu hueneza magonjwa yanayosababishwa na virusi au bacteria.

7.5 Kuondoa Majani
Ondoa majani yote yanayoonyesha dalili za magonjwa au kushambuliwa na wadudu na yale yote
yaliyozeeka ili kupunguza hali ya unyevu na kuruhusu hewa ya kutosha kwa mimea.
Ondoa majani mawili au matatu yaliyo chini ya ngazi ya kwanza ya matunda kisha yachome au yafukie

7.6 Kukata Kilele
Kwa kawaida aina ndefu ya nyanya huzaa ngazi zaidi ya sita za matunda, lakini mmea una
uwezo wa kubeba ngazi tano hadi sita tu.
Hivyo ni muhimu kukata sehemu ya juu ya mmea (kilele) ili kusimamisha ukuaji wake.
Kata kilele mimea ifikiapo ngazi hizo.
Jani moja liachwe juu ya ngazi ya mwisho (ya tano au ya sita).

Machipukizi yote yanayojitokeza pembeni hayana budi kuondolewa ili kupata matunda
makubwa na yatakayoiva upesi.

7.7 Palizi

Palizi katika shamba la nyanya ifanywe kwa uangalifu ili kuepuka kukata mizizi.
Punguza palizi ya mara kwa mara kwa kuweka matandazo kuzuia uotaji wa magugu.
Wakati wa kupalilia, pandishia udongo kwenye shina.

7.8 Kumwagilia Kwa kawaida nyanya hutoa mavuno mengi wakati wa kiangazi kuliko wakati wa masika. Mwagilia maji ya kutosha mara mbili kwa wiki hasa matunda ya kwanza yanapoanza kutunga.
Kumwagilia maji mengi sana au kidogo sana kunasababisha matunda yawe na hitilafu ya
kupasuka.
Wakati wa mwanzo epuka kumwagilia maji mengi ili mimea isididimie.

7.9 Kuweka Mbolea ya Kukuzia
Mbolea ya kukuzia huwekwa mara mbili.
Mara ya kwanza weka gramu tano za S/A auCAN kwa
kila mche katika wiki ya pili hadi ya nne baada ya kupandikiza.
Rudia tena kuweka kiasi hicho
hicho wakati matunda ya ngazi ya kwanza yanapoanza kuiva.


8.0 MAGONJWA NA WADUDU

8.1 MAGONJWA YA NYANYA

8.1.1 Bakajani chelewa (Late blight)

Ugonjwa huu huenenzwa na vimelea vya fangasi.
Husababishwa na hali ya hewa hasa ya unyevunyevu , ukungu , huenezwa na upepo. Majani, shina na matunda hushambuliwa.

Dalili za ugonjwa huu huanza kuonekana kwenye jani la chini. Majani na shina huwa na mabaka
makubwa yenye rangi nyeusi au kikahawia nzito.
Katika sehemu zenye hali ya hewa ya
unyevunyevu, majani huoza na hatimaye ukungu mweupe na kijivu huonekana chini ya jani.
Majani haya baadaye hukauka na kuwa kama yaliyounguzwa na moto. Mashina pia huwa na
mabaka ya kikahawia.
Matunda yaliyopatwa na ugonjwa huu huwa na madoa ya rangi ya kijani
iliyochanganyika na kikahawia. Baadaye madoa haya huwa makubwa na hatimaye huoza. Ukipasua tunda lililoathiriwa utaona weusi.
Nyanya zenye ugonjwa huu zikihifadhiwa kwenye
sehemu yenye unyevu mwingi hutoa ukungu mweupe.

Udhibiti

Nyunyiza dawa ya kuzuia ukungu hasa wakati wa masika,

Dawa zinazopendekezwa ni
Ridomil, Dithane 45, Bravo, Funguran, milraz, Topsin M 70, Cupric Hydroxide
(Champion) na Copper Oxychloride (Cupro).


Contact
kimariyogeofrey@gmail.com

Comments

Popular posts from this blog

UFUGAJI BORA WA NGURUWE

UFUNGAJI WA KUKU WA MAYAI

KILIMO CHA VITUNGUU